To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com                                                 To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com

Tuesday, 15 March 2011

TAARIFA KWA WATANZANIA WALIOKO JAPAN!!


TAARIFA KWA WATANZANIA WALIOKO JAPAN.

Kufuatia majanga ya tetemeko na tsunami yaliyoikumba Japan tarehe 11 Machi, 2011, na matetemeko yanayoendelea (aftershocks), Ubalozi unapenda kuchukua nafasi hii kutoa pole kwa Watanzania na wananchi wa Japan waliokumbwa na misukosuko hiyo na kwa madhara yaliyotokana na majanga hayo. Kama ilivyoonyeshwa katika taarifa mbalimbali, maisha na mali nyingi za watu zimepotea, hususan wale waliopo mikoa ya Miyagi, Fukushima, Iwate na maeneo mengine.

Hali ya Usalama wa Watanzania wanaoishi Japan
Kwa ujumla ubalozi umekuwa ukifuatilia hali ya usalama ya Watanzania kwa ujumla tangu majanga hayo yalipotokea kwa kuwasiliana na Watanzania waliopo maeneo mbalimbali, jumuiya ya Watanzania na mamlaka ya Serikali ya Japan. Mpaka sasa taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba Watanzania wote, hata wanaoishi katika maeneo yaliyokuwa na hatari zaidi wapo salama.

Endapo kuna Mtanzania ambaye ana taarifa muhimu kutokana na janga hili ni vyema akawasiliana na Ubalozi ili kutuwezesha kuchukua hatua stahiki. Ni vizuri kila Mtanzania akafahamu kuwa Ubalozi utaendelea na kazi ya kutafuta na kutoa taarifa kwa wananchi wake kwa jinsi unavyoendelea kuzipokea kutoka mamlaka ya Serikali husika. Kwa kufanya hivyo kutasaidia kuondoa uwezekano wa kutoa taarifa ambazo zitapingana na taarifa za Serikali ya Japan. Hivyo ni vyema kwa Watanzania kuwa na subira na usikivu, ili wote tuweze kuvuka salama.

Tahadhari kuhusu Mitambo ya Nuclear
Ubalozi unawasihi Watanzania waliopo katika maeneo ambayo tahadhari bado zinaendelea kutolewa kama Fukushima na maeneo mengine yaliyo karibu na Mitambo ya Nuclear Reactors kuendelea kusikiliza na kufuatilia kwa makini taarifa na maelekezo muhimu yanayoendelea kutolewa na Serikali ya Japan, ikiwa ni pamoja na kuondoka katika maeneo yote ambayo ni hatari na kwenda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya usalama wao.

Taarifa ya Mgao wa Umeme
TEPCO wametangaza Mgao wa Umeme (rolling blackout) kuanzia tarehe 14 Machi, 2011 katika maeneo ya Tokyo pamoja na mikoa ifuatayo; Gunma, Tochigi, Ibaraki, Saitama, Chiba, Kanagawa, Shizuoka na Yamanachi. Kata zitakazoathirika ni Taito, suginami, Shinagawa, Meguro, Ota, Setagaya, Toshima, Kita, ArakawA, Itabashi, Nerima, Adachi na Katsushika. Miji yote 26 ya Tokyo na Tama-gun nayo itaathirika pamoja na baadhi ya maeneo jirani na miji hiyo. TEPCO wametoa ratiba kamili katika Tovuti yao.

Serikali ya Japan inawaomba wakazi wote kupunguza matumizi ya umeme kadri inavyowezekana na kutosafiri nje ya maeneo yao kama hakuna ulazima wa kufanya hivyo, hususan kwa wanaoishi maeneo ya mikoa iliyotajwa, ili kukabiliana na upungufu uliopo. Vilevile, Serikali imetahadharisha uendeshaji wa magari kwa vile alama nyingi za barabarani zitakuwa hazifanyi kazi.

Kwa sababu ya mgao wa umeme treni nyingi na sub-ways Jijini Tokyo zitapunguza huduma. Tafadhali angalia tovuti za treni au njia za treni husika ili kujua ratiba zake mpya.

Usafiri wa Anga
Ubalozi unapenda kuwataarifu kuwa endapo kuna ndugu au jamaa yeyote anayetarajia kusafiri kuja Japan kusitisha safari hizo hadi hapo Serikali ya Japan itakapotoa taarifa za kutengamaa kwa hali hii inayoendelea hivi sasa. Aidha, kutakuwa na uchelewesho wa kuruka kwa ndege kutoka viwanja vya ndege vya Narita na Haneda, kwa wale wanaotarajiwa kusafiri kwa njia hiyo. Tafadhali wasiliana na Shirika unalosafiri nalo kwa taarifa zaidi.

Misaada
Ni vyema pia ikafahamika kuwa suala la kutoa misaada kwa Serikali ya Japan kufuatia janga hili ni suala la Kiserikali na haliwezi kufanywa na mtu mmoja mmoja kama wengine tunavyodhani. Ziko njia sahihi za kutekeleza suala hili na taratibu zinafanyika.

Mawasiliano kwa ajili ya utoaji na upatikanaji wa taarifa mbalimbali

Pamoja na taarifa hii pia Ubalozi unapenda kutoa njia mbalimbali za mawasiliano zilizotolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya kupata taarifa za maafa, kutafuta waliopotea, na taarifa za tahadhari;

Kwa mawasiliano na Ubalozi tafadhali tumia namba za simu na email address zifuatazo:

090-9814-5959 Francis Mossongo, fmossongo@tanzaniaembassy.or.jp
080-35194229- Mrs. Jilly Maleko Jmaleko@tanzaniaembassy.or.jp

Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania
Japan
14Machi 2011

No comments: