To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com                                                 To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com

Wednesday, 9 February 2011

Maggid na tafsiri yake,sakata la wabunge wa chadema kutoka nje ya bunge!!

copyright;maisha blog
Ndugu Zangu,


SASA ni dhahiri shahiri kuwa CHADEMA inapoteza mwelekeo. Hili si jambo jema kwa demokrasia yetu changa tunayotaka kuijenga. 

Nimesoma kwa makini magazetini habari kuhusu sakata la wabunge wa CHADEMA kutoka nje ya ukumbi wa Bunge jana jioni. Hakika sikuona mantiki wa walichokifanya mbali ya CHADEMA kuanza kutengeneza ombwe la upinzani wenye maana uliotarajiwa na Watanzania wengi. 

Miezi mitano imepita tangu tumalize uchaguzi, CHADEMA bado hawaonekani kufunga ukurasa wa siasa za wakati wa kampeni za uchaguzi. CHADEMA wana lazima ya kuingia kwenye maisha magumu na ya kawaida ya kisiasa.

Maisha ya kisiasa yenye changamoto zake. Migogoro ya ndani ya Chama ikiwamo kutofautiana kimawazo. Uimarishaji wa chama mikoani na wilayani, kwa nchi nzima na mengine mengi. Ni ukweli CHADEMA bado haijaimarika katika ngazi za chini. 

Na changamoto za kisiasa hazikimbiwi, hukabiliwa kwenye majukwaa ya kisiasa. Wabunge wa CHADEMA hawakuwa na sababu za msingi za kutoka nje ya bunge. Badala yake, wangepambana kwa hoja ndani ya Bunge. CHADEMA si wanajua, kuwa hatma ya jambo lile lilikuwa ni kupigiwa kura. Kwamba wangeshindwa. Ni sehemu ya mapambano ya kisiasa. 

Watanzania tuna matatizo haya mawili; Mosi, tu mahodari sana wa kuukana ukweli. Pili, tu mahodari sana wa kuupotosha ukweli. Ukichanganya na kukimbilia kushabikia mambo na kutofikiri kwa kina, basi, tunashindwa kabisa kuambizana ukweli hata kama tunauona. Kwa kitendo cha jana, Wabunge wa CHADEMA hawakuwa sahihi. Kuwaambia vinginevyo si kuwasaidia.

Wakati mwingine kukimbilia kutoka nje ya Bunge hakupelekei kupata huruma ya kisiasa bali hasira za kisiasa kutoka kwa wapiga kura. Ndio, kuna gharama zake. Mtatotaka nje bungeni mara ngapi? Na CHADEMA kutoka nje bungeni kulikuwa na hasara zaidi kuliko faida. Huku mitaani, kuna watu wanaoanza kuiangalia CHADEMA kwa miwani mingine. Kwa staili hii, itafika mahali Wabunge hao wakaja kuzomewa Kibaigwa, Msamvu na kwengineko.


Na David yule wa Kafulila kausema ukweli wake; kuwa. "Tunashinda kwa asilimia 20 tunakataa mseto, tukipata asilimia 60 hali itakuwaje, ukipata kidogo uoneshe una busara ya kufanya kazi pamoja, kwa hali hiyo ukipewa kikubwa huwezi kuaminika." Anasema David Kafulila wa NCCR Mageuzi.

Sikilizeni, enyi ndugu zangu wa CHADEMA, yale tuliokuwa tukiwashutumu CCM, CHADEMA sasa mnayafanya mara mbili yake! Tumeilaumu, na bado tunailaumu sana CCM kuwa chama kisichokubali mabadiliko. Chama ambacho hakitaki kujenga misingi ya kugawana madaraka na wengine. 

Leo CHADEMA hamjaingia madarakani mnaanza mapema kuwachagua wa kukaa meza moja na nyinyi. Mnavikebei vyama vingine ikiwamo CUF. Tuchukue mfano wa CUF, badala ya kuwakebei, busara ingekuwa kuwapa heshima yao stahiki kwa mchango wao wa kuleta mageuzi ya kisiasa hapa nchini.

Inapofika mahali idadi ya wapiga kura wote wa wabunge wa Zanzibar inapofananishwa na idadi ya wapiga kura wa jimbo la John Mnyika la Ubungo, na kuwa kigezo cha mbunge wa kutoka Zanzibar asiwe Mwenyekiti wa Kamati ya bunge, basi, hapo kuna tatizo maana, tutakuja kuambiwa Rais wa nchi hii hawezi kutoka Zanzibar maana huko watu wake hawazidi milioni moja!

Hakika, huu ni wakati wa CHADEMA na wabunge wake kutanguliza busara. Huko tunakokwenda tungependa tuwe na serikali za mseto. Na CHADEMA wana nafasi ya kuonyesha mfano wa kunyosha mkono wa ushirikiano na vyama vingine vya upinzani bungeni, hata viwe vidogo kiasi gani. Waonyesha utayari wa kushirikiana na kuvishirikisha vyama vingine vya upinzani badala ya kuvipa mgongo. Inawezekana.

Maggid
Iringa,

source:mjengwa.blogspot.com

No comments: