To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com                                                 To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com

Wednesday 8 June 2011

IKULU YA HUZUNISHWA NA KAULI YA VIONGOZI WA DINI....


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa za Maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kumpa Rais Jakaya Mrisho Kikwete saa 48 kuwataja kwa majina viongozi wa dini wanaotuhumiwa kujihusisha na madawa ya kulevya, ni kauli ya kusikitisha na ambayo haikutegemewa kutoka kwa viongozi hao wa dini.
Viongozi wa dini ni watu wa kutumainiwa sana katika jamii yeyote, lakini ikizingatiwa kuwa wao sio malaika ama watakatifu hapa duniani, kwani nao wanatumbukia katika majaribu na kujikuta katika vitendo au hali isiyo tegemewa kabisa.
Katika Hotuba yake kwenye sikukuu ya kuwekwa wakfu na kusimikwa Mhashamu Askofu John Ndimbo kuwa Askofu wa Jimbo la Mbinga, Rais Kikwete alitoa ombi ambalo si geni kwani alishalitoa katika hafla zingine pia zilizohusisha viongozi wa dini. 
Katika sherehe hiyo Rais alitoa ombi la kuwataka viongozi wa dini wajihusishe kwa ukamilifu katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Rais Alisema, “Ni tatizo linalozidi kukua pamoja na jitihada za Serikali kupitia vyombo vya usalama kuwabana, kuwawajibisha watumiaji na wafanyabiashara ya dawa za kulevya. Athari zake kwa jamii zinaeleweka hivyo haihitaji kuzirudia”
Rais alieleza, “Hata hivyo niruhusuni niseme tu kwamba tusipofanikiwa kulidhibiti tatizo hili, hasara yake ni kubwa mno. Watoto wetu wengi wataharibika, uhalifu, hasa wa wizi na mauaji utaongezeka. Taifa litaharibikiwa.” Amesema Rais na kuendelea kueleza kuwa, “Siku hizi kila siku kuna watu wanaokamatwa kwa kujihusisha na dawa za kulevya. Inaashiria kuimarika kwa vyombo vyetu vya usalama, Lakini inasikitisha sana kuona kuwa biashara hiyo sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu.
Huku sasa tunakoelekea kwa kweli ni kubaya sana.Mimi Nawaomba mtoe uzito unaostahili kwa tatizo hili. Viongozi wa dini mnasikilizwa, Nawaomba kemeeni, onyeni na elimisheni jamii juu ya madhara ya dawa za kulevya, waelimisheni vijana ambao ndiyo walengwa wakuu, waepuke na waache kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya”. Rais alisema.
Kwa maneno haya, tunategemea viongozi wa dini kuchukua onyo hili la Rais kama ishara (Clue) na kuanza kuifanyia kazi.
 Mtu akikuonya kuwa nyumbani kwako kumeonekana nyoka, huanzi kwa kuuliza kama kweli, ni wa rangi gani? Unatakiwa kushtuka na kuweka na kujiandaa kumsaka kwa nia ya kumuondosha nyumbani kwako hata ikibidi umuue ili asije akaleta madhara makubwa kwako na kwa familia yako. Rais ana nia njema sana katika kulielezea jambo hili na mwenye nia njema haumbuki.
Hivi karibuni wapo viongozi wa dini wamekamatwa kwa rushwa, ngono na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo mbalimbali ambavyo ni kinyume na maadili yasiyotegemewa na jamii kwa ujumla, wapo ambao wameshakamatwa na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria, wapo wanaochunguzwa, tumeshawashuhudia na bado wataendelea kushuhudiwa. Hili si jambo dogo la kujitetea kwa kauli nyepesi kutoka kwa watu wanaotegemewa na jamii kwa kumpa Rais saa 48. 
Anaejishuku ajisalimishe mwenyewe, anaeshukiwa na jamii afichuliwe ili afanyiwe uchunguzi na hatimaye sheria ichukue mkondo wake lakini msisubiri Rais awataje hadharani ndiyo muanze kuchukua hatua.
Mnategemewa muweke mikakati na vipaumbele vya kufanyia kazi changamoto hiyo, na sio kuaihirisha tatizo hili ambalo linazidi kuwa kubwa. Kazi hii ya kupambana na madawa ya kulevya haimhusu Rais peke yake inamhusu kila Mtanzania, popote alipo katika nafasi yake na viongozi wa dini wananafasi kubwa sana kwa sababu wao wanasikilizwa, wanatoa ushauri na wanategemewa kuwa na maelekezo yanayompendeza Mungu.
Imetolewa na: Premi Kibanga
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi Ikulu,
Dar es Salaam. Juni 07, 2011.

3 comments:

Goodman Manyanya Phiri said...

Siku hizi kusema ukweli dini hayipo katika ile mikusanyiko ya watu wanaojidai ni wenye dini!


Ni ukweli kabisa aliyeyasema Rais Kikwete: wapo viongozi wa dini wa bovu kiasi cha kutembeza madawa ya kulevya hata kwetu hapa Afrika Kusini wapo tu (pamoja na mahubiri yao ya moto moto).


Hiyo siyo siri; labda iwe siri kwa mtu alielewa madawa ya kulevya aliyekuwa anawasafirishia watoto waMungu kwenye kanisa au msikiti wake!


Kasoro ni moja, lakini, katika POST yako, Mkuu Mkandawile: mbona hutuonyeshi ile kauli au FULL STATEMENT ilietolewa na viongozi wa dini? Tusipoyiona, tunaweza tukawa tunakosea kutoa maoni ya maana; tunaweza tukapendelea upande mmoja bure!


Ukweli kabisa ni kwamba SPEECH nzima ya Rais tuisome; vilevile SPEECH/STATEMENT nzima ya viongozi wa dini tuisome pia bila kutegemea HEARSAY ya huyu Mheshimiwa serikalini ya Kikwete.



Unajuwa, hawa tembo wawili (dini na dola) wakipigana, tunaumia sisi hapa! Maana yake sisi walala hoi tunampenda Rais wetu yoyote yule hapa kwetu, Afrika. Vilevile tunawapenda viongozi wetu wa dini, kwani sio wote wabovu http://www.telegraph.co.uk/news/worldnews/1562824/Mugabe-boost-as-adulterous-bishop-resigns.html.

Raymond Mkandawile said...

Kaka Phili najitahidi sana kutafuta tamko lao na mara nikilipata mitakupa link yake,however viongozi hao wametoa kauli mbalimbali kwenye vyombo vya habari kana kwamba wamedhalilishwa na kauli ya Mh.Rais..japo swari linabakia kuwa je hawa watu ni maraika?na je ni kweli makanisani mambo hayo hayafanyiki?kama siyo na viongozi je waumini wote ni safi na hawajihusishi na biashara hiyo?na je kulikuwa na sababu gani ya wao kuamua kujibu badala ya kulifanyia kazi swala hilo?
Inashangaza lakini sishangai kwani zote hizo zinaonyesha kwamba ni siku za mwisho kaka Manyanya..."Ukiambiwa kuna nyoka nyumbani mwako usiulize ana rangi gani bali tafuta jinsi ya kumuua"

Goodman Manyanya Phiri said...

Tuko pamoja kabisa, Mkuu, kimawazo hapo!