To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com                                                 To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com

Friday 27 April 2012

RAY ANENA JUU YA KIFO CHA SWAIBA WAKE KANUMBA..



Ikiwa ni tariban mwezi sasa umepita tangu msanii maarufu wa filamu, Steven Charles Kanumba afariki dunia, msanii mwenzake Vincent Kigosi ‘Ray’ ameamua kuandika waraka mzito kueleza kwa nini hahusiki na kifo cha swahiba wake huyo kama ambavyo imekuwa ikisambazwa na watu wasiomtakia mema.

Waraka huo ulinaswa hivi karibuni kupitia blogu yake ambapo baada ya timu ya gazeti hili kuupitia ikaona ni vyema ukasomwa na Watanzania wote ili kuweza kupata jibu la kwa nini yeye hahusiki? Waraka huo ni huu hapa chini…

******************

Yapata wiki tatu sasa tangu msanii mwenzangu Steven Kanumba aage dunia na kama ilivyo kwa kila kitu kinapotokea huandamana na kila aina ya maneno na hisia mbalimbali kutokana na mitazamo ya watu kupishana kuhusiana na jambo husika. 

Kulingana na muktadha huo, msiba wa Steven Kanumba umekumbwa na maneno na hisia kama hizo, hususan mazingira ya kifo chake. Kinachosikitisha zaidi watu wengi (ambao wanajitambulisha kama wapenzi wa Kanumba) na baadhi ya vyombo binafsi vya habari vimekuwa vikinihusisha na kifo hicho kwa kusema kwamba kwa njia moja au nyingine nahusika na mauaji ya Steven Kanumba. 

Kwa muda wote huo tangu msiba ulipotokea mpaka leo hii nashika kalamu kujaribu kuyaweka sawa na kuondosha hisia chafu katika fikra za watu. Nimekuwa nikipitia katika wakati mgumu sana kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikinyooshewa vidole kila upande nikihusishwa na kifo hicho.

Kiujumla nimezingatia maoni ya wapenzi na mashabiki wangu wakinitaka kuwa na subira ila kuna usemi usemao, uongo ukirudiwa sana jamii huusadiki na kuuona ukweli, nimeona nisikae kimya ila niweke sawa hili kwamba sihusiki na kifo cha Steven Kanumba.
Nasema wazi kwanza sihusiki kabisa na kifo cha Kanumba kwa kuzingatia mazingira yenyewe ya kifo kilivyotokea. Wakati kifo hicho kinatokea, nilikuwa sehemu nyingine kabisa na mimi nilikuwa mtu wa tatu kutaarifiwa kwamba Kanumba amepatwa na mkasa ambao baadaye ulisababisha kifo chake. 
Hata nilipofika katika Hospitali ya Muhimbili (tofauti na watu wanavyodhani kuwa nilifika nyumbani kwake, ukweli mimi nilimkuta tayari amepelekwa Muhimbili), nilikuta tayari alikuwa ameshafariki ndiyo maana hata polisi wanaohusika na usalama wa raia, si tu kwamba hawakuniweka chini ya ulinzi, sikuitwa hata kuhojiwa kwa sababu hakuna mazingira yoyote yanayonihusisha mimi na kifo hicho.
Pengine watu wanaojaribu kuongea hayo, hawajui mimi na Steven Kanumba tumetoka wapi? Sisi si watu tuliokutana barabarani, tuna historia katika kazi yetu ya sanaa na pia katika maisha  yetu. Mwanzoni kabisa, mimi ndiye niliyempokea Kanumba pale Kaole na ndiye niliyemfundisha sanaa pale (nadhani watu wanakumbuka tamthiliya za wakati huo ITV).
Baada ya hapo tulienda pamoja katika Kampuni ya Game 1st Quality na tukafanya filamu kama Johari, Sikitiko Langu, Dangerous Disire na nyinginezo na tuliendelea kuwa pamoja katika kampuni hiyo mpaka tulipofanya filamu ya Oprah mwaka 2008 ambapo niliingia rasmi kufanya kazi za kampuni yangu, lakini tuliendelea kuwa pamoja hata wakati nikiendelea na kazi za kampuni yangu. 
Pia mimi nilikuwa wa kwanza kuanza kufanya kazi na Steps na baadaye Kanumba alipoanza kufanya kazi zake mwenyewe na kunikuta huko tuliendelea kuwa pamoja kama siku zote. Kitu kikubwa kilichokuwa kinaendelea baina yetu ni kwamba tulijenga ushindani wa kuendeleza kazi mbele kwa kila mmoja akitoa kazi, mwingine anamjibu.
 Isitoshe hata vitu vyetu binafsi utaona kama kuna kufanana. Kuna wakati Kanumba alinunua Toyota Rav 4 nyeusi mimi nikanunua ya kijani, aliponunua Harrier na mimi nikanunua pia na hata gari za hivi karibuni, ukitazama utaona kuwa zinafana kwa karibu. Hii ilikuwa ni kama maisha yetu, hatukuwa na uadui, ilikuwa tunapeana changamoto za maendeleo.

Watu wanaojaribu kuonesha kuwa tofauti zetu ilikuwa ni uadui, huwa hawajui wapi tulikotoka ndiyo maana wanasema wasemavyo na katika kuthibitisha kuwa tofauti hizo hazikufikia katika uadui, kuna watu ambao wanafanya kazi nami katika kampuni yangu ya RJ ndiyo hao hao Kanumba alikuwa anawatumia siku zote katika kazi zake, hata baada ya tofauti hizo hakuna aliyekoma kufanya kazi na yeyote kati yetu. 

Kumtuhumu mtu kwa namna yoyote ile bila ya uthibitisho wa tuhuma hizo, ni kosa kwa sheria za nchi na pia kama ni mfuasi wa dini yoyote ni dhambi, kwani wakati ukisema hayo huku hujui uhalisia bali unasukumwa na nguvu za hisia tu ni sawa na kumchafua mtu huyo katika jamii bila ya kujua jamii inamchukuliaje.

Napenda kusema wazi kuwa, kwa kila anayetekwa na wimbi hili, ajaribu kufikiria leo ipo kwangu mimi, kesho inaweza kuhamia kwako, kwani mimi siyo wa kwanza kufikwa na haya. Inaweza kukukuta hata wewe au ndugu yako, utajisikiaje!

Na kama kweli mimi nimehusika na kifo cha Kanumba kwa namna yoyote ile, basi Mungu atanihukumu na kila aliye hai atashuhudia ila kama sijahusika kwa lolote, Mungu hatonihukumu na badala yake ataniinua kwa kuwa ninapita katika kipindi kigumu mno sasa hivi kwa madhira haya.

Mwisho kabisa napenda kumaliza kwa msemo usemao, ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke kwani kadiri mambo haya yanavyoendelea, usidhani yataishia kwangu, kwani mkono wa dhuluma hauishii karibu, ukisikia jirani anapiga kelele za mwizi, usilale nenda kamsaidie.

Usiseme kuwa hatuhusiki kwani hayupo kwetu, kesho utafikwa na wewe utakosa wa kukusaidia. Cha msingi kama tunampenda sana ndugu yetu ni kumuombea kwa Mungu, kwani hatujui makao yake huko aliko na siyo kuunda vitu ambavyo kamwe hata yeye angekuwa hai asingeviafiki.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU STEVEN KANUMBA MAHALI PEMA

PEPONI -AMINA.


No comments: