To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com                                                 To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com

Wednesday, 9 February 2011

Chadema wasusa kikao kingine Bungeni!!

copyright;maisha blog

Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana jioni walisusa kuipitisha au kuikataa hoja ya kuifanyia marekebisho Kanuni ya 14 ya Bunge, wakatoka nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma. 
Kanuni hiyo inazungumzia muundo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni ili kuviwezesha vyama vyote vya upinzani bungeni kuunda kambi rasmi, baada ya kuwasilishwa kwa Spika na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR- Mageuzi) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF). 

Wabunge hao wakiongozwa na kiongozi wao, Freeman Mbowe, walitoka ukumbini baada ya Mbowe kuchangia hoja hiyo. Mbowe aliipinga hoja hiyo, na mara baada ya kumaliza kuzungumza, aliwaongoza wenzake kutoka ukumbini. 

Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, alikiponda kitendo hicho cha wabunge wa Chadema na kuhoji kama watakuwa wakifanya hivyo kila wanapopinga hoja zinazowasilishwa bungeni. 

Mjadala wa jana ulikuwa mtihani wa kwanza kwa Spika Makinda, katika kudhibiti nidhamu ya Bunge jipya la 10, lililoanza vikao vyake mjini hapa jana kwa baadhi ya wabunge kutoleana maneno ya kejeli, maudhi, vijembe na lugha zilizotafsiriwa kuwa za matusi. 
Hali hiyo ilijitokeza wakati wabunge wakijadili Bunge lililazimika kuijadili hoja hiyo kupitia Kamati ya Kanuni za Bunge 

iliyoundwa na Spika Makinda, kabla ya maazimio yake kuwasilishwa katika kikao cha Bunge jana na Naibu Spika Job Ndugai, ili kupata uamuzi wa wabunge wote. 

Akisoma maazimio ya Kamati ya Kanuni za Bunge, Naibu Spika Ndugai, alisema baada ya kukutana juzi jioni, Kamati hiyo ilijadili kwa kina hoja za wabunge na 
Kafulila na Hamad na kubaini kuwa ni kweli kulikuwa na kasoro katika fasili ya 
11 ya kanuni za Bunge kifungu namba 113 toleo la mwaka 2007, juu ya tafsiri 
ya neno kambi rasmi ya upinzani bungeni. 
Ndugai alisema, kwa vile wabunge Kafulila na Hamad waliomba hoja zao kufanyiwa kazi mara moja kabla ya uteuzi wa wenyeviti wa kamati za kusimamia fedha za umma ambao ni lazima watoke kambi ya upinzani, Spika aliona ni busara suala hilo likajadiliwa mara moja na kupatiwa ufumbuzi ili kuepusha nafasi hizo kuchukuliwa na chama kimoja tu cha Chadema, ambacho kilikuwa kinatambuliwa kama kambi rasmi ya upinzani bungeni. 

Alisema, katika uamuzi wake, Kamati ya Kanuni za Bunge ilibaini kuwa kulikuwa na utata katika tafsiri ya neno kambi rasmi ya upinzani bungeni, katika kanuni 
namba 14, 15 na 16 za Bunge, hatua iliyoifanya Chadema kudhani kuwa kwa vile imetimiza asilimia 12.5 ya wabunge bungeni, basi inaweza kuunda kambi 
rasmi ya upinzani bungeni peke yake. 

Alisema kutokana na kubaini hilo, Kamati hiyo ilipendekeza neno rasmi lipewe 
maelezo ya ufafanuzi, ili isomeke kuwa kambi rasmi ya upinzani bungeni ni ile 
inayoundwa na vyama vyote vya upinzani ndani ya Bunge kwa mujibu wa 
fasili ya 2 ya kanuni ya 14 ya Bunge. 

Alisema kazi nyingine iliyofanywa na Kamati hiyo ilikuwa ni kuyafanyia 
marekebisho majina ya Kamati za Kudumu za Bunge ili ziweze kuendana na wizara mpya zilizoundwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni. 

Baada ya Naibu Spika kutoa hoja hiyo, wabunge walipata nafasi ya kuijadili 
lakini katika hatua isiyotarajiwa, baadhi ya wabunge walionekana kutumia jazba, vijembe, kejeli na lugha za maudhi, hatua iliyosababisha nidhamu ya Bunge kutetereka na kumfanya Spika kulazimika kuingilia mara kwa mara mijadala ya wabunge au wabunge wenyewe kukinzana. 

Akichangia hoja hiyo, Kafulila alisema lengo la marekebisho husika ni kuifanya 
kambi ya upinzani kufanya kazi pamoja, ili kuleta umoja na mshikamano na 
kuidhibiti Serikali iliyopo madarakani, dhidi ya serikali inayosubiri kuingia 
madarakani. 
“Mheshimiwa Spika hii ni aibu sana, mimi napata hofu kama kiongozi aliyepata 
asilimia 20 tu ya ushindi, anaanza kuwabagua wenzake, hivi itakuwaje siku akipata ushindi wa asilimia 60? Kama hali imekuwa hivi katika kidogo kilichopatikana, itakuwaje siku tukipata kikubwa?” alihoji. 

Kwa upande wake, Hamad alisema anasikitika kuona Chadema imeanza ubaguzi dhidi ya vyama vingine vya upinzani, baada ya kupata asilimia kubwa katika uchaguzi uliopita, wakati katika Bunge la Tisa, CUF ilikuwa na idadi kubwa ya 
Wabunge, lakini ilishirikiana na vyama vingine vya upinzani kuunda kambi rasmi 
ya upinzani bungeni. 
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alisema lengo la marekebisho hayo ni kutaka kuua upinzani bungeni na kuihujumu kambi ya upinzani bungeni, kwa vile itakuwa vigumu kwa kiongozi wa upinzani bungeni kujenga nidhamu kwa wabunge wanaotoka vyama vingine vya upinzani, kutokana na tofauti ya mtazamo na itikadi. 
Hata hivyo, mchango wa Mbunge huyo ulionekana kukatizwa mara kwa mara na Spika Makinda na wabunge wa CCM na vyama vingine, kutokana na kauli zake nyingi kudaiwa kuwa za uongo, maudhi au matusi ambapo pamoja na kubanwa na Spika ili afute kauli hizo, Mdee alikaidi kwa muda kabla ya kufuta kauli zake na wakati mwingine kuzirudia. 

Mfano mzuri ni pale Spika alipolazimika kumkatisha Mdee na kumwelekeza mchakato wa muundo wa kambi ya upinzani bungeni ulivyokuwa tangu kuanza kwa vyama vingi vya siasa nchini, lakini baada ya Spika kumaliza, Mdee alimwambia kwamba alichokuwa anakisema ni kama hicho kilichosemwa na Spika na hivyo alikuwa amempotezea muda wake. 

Kauli nyingine ni pale Mdee aliposema CUF ni CCM B na hivyo inataka kuua 
upinzani, kauli iliyopingwa na Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Ruvuma, Stella Manyanya (CCM) aliyetumia kanuni ya 64 kuliambia Bunge kwamba Mdee alikuwa ametumia lugha ya maudhi. 

Alifuatia Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), ambaye aliunga mkono marekebisho hayo akisema yatajenga umoja na mshikamano kwa vyama vyote vya upinzani bungeni. 

Hata hivyo, nidhamu ya Bunge ilitetereka tena alipoinuka Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), ambaye aliipinga hoja hiyo, kwamba inakiuka desturi, kanuni na mila za mabunge ya Jumuiya ya Madola, ambayo yanatamka wazi, kwamba chama kinachopata asilimia kubwa ya kura kinaunda Serikali huku kinachofuatia kwa wingi wa kura kikitakiwa kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni ili kudhibiti fedha za umma. 

Wakati Lissu akizungumza, baadhi ya wabunge wa CCM walikuwa ama wakimkatiza kwa sababu mbalimbali kama kuomba mwongozo wa Spika na hata kutoa taarifa kwa Spika, lakini wakati mwingine walikuwa wakizomea na kuzungumza katika vipaza sauti wakitoa lugha ya kejeli na vijembe, hatua iliyomfanya Spika naye kusimama mara kwa mara kutoa mwongozo. 

Aliposimama Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM), pamoja na kuunga mkono hoja hiyo, alimtaka Spika Makinda kuzisimamia vilivyo kanuni za Bunge akisema kulikuwa na dalili mbaya za kulifanya Bunge kuwa kijiwe na kuomba kanuni za Bunge kutazamwa upya. 

Tukio la kusitikisha zaidi ni lililotokea wakati Lissu akizungumzia kwamba 
Cheyo asingeweza kusimamia ipasavyo Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa vile chama chake, UDP kina Mbunge mmoja tu, kauli iliyomfanya Cheyo kuhamaki na kuzungumza maneno makali dhidi yake kwa kumtaka kufunga mdomo akisema mbona huko nyuma aliweza kufanya vizuri. 

Hoja hiyo ilitarajiwa kupigiwa kura jana jioni ili kupitishwa ama kutopitishwa 
ingawa kulikuwa na dalili za wazi za kuungwa mkono kutokana na idadi kubwa ya wabunge wa CCM na vyama vya upinzani isipokuwa Chadema, kuiunga mkono kwa kila hali.
source:habari leo.

No comments: