To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com                                                 To Advertise on this Blog please Call: +255 (0)656 56 13 14 or Email: maishablog@yahoo.com

Wednesday, 13 April 2011

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAKATI WA MISA YA KUMBUKUMBU YA MIAKA 27 YA KIFO CHA HAYATI EDWARD MORINGE SOKOINE ILIYOFANYIKA KATIKA KANISA KUU LA MT. PAULO WA MSALABA MJINI DODOMA TAREHE 12 APRILI 2011 
waziri mkuu mh.Mizengo Pinda.
Siku kama ya leo, tunapokutana kuadhimisha Kumbukumbu ya Kifo cha Mpendwa wetu, Mzee Edward Moringe Sokoine inakuwa vigumu sana kupata maneno mazuri ya kusema. Inakuwa vigumu kwa sababu ukweli hatuko naye tena, lakini kwa njia moja ama nyingine tunaamsha hisia zetu na upendo wetu tuliokuwa nao kwake na ambaye sasa ametutangulia mbele ya haki.
Faraja ninayoipata Mimi kama Pinda, kwa siku ya leo tunapoadhimisha kumbukumbu kama hii ni kuwa bado huyu mwenzetu tuko naye kimawazo, kiakili na kubwa zaidi kiroho.
Vilevile, kwa mawazo yangu, na kwa kuamini kwangu, siku ya leo ni muhimu kwa kuwa inatukumbusha kuwa sote hapa duniani ni wapita njia na siku moja tutaungana na waliotutangulia mbele ya haki huko Mbinguni.
Leo tunatimiza miaka27 tangu Marehemu Edward Moringe Sokoine atutoke gafla kwa ajili ya gari. Mtakumbuka kwamba Marehemu Sokoine alikuwa Waziri Mkuu kwa vipindi viwili tofauti. Alikuwa Waziri Mkuu wa Tatu wa Tanzania baada ya Marehemu Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Rashidi Mfaume Kawawa.
Alianza kuwa Waziri Mkuu tarehe 13 Februari 1977 hadi 7 Novemba 1980. Baadae tena aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha pili tarehe 23 Februari 1983 hadi 12 Aprili 1984 alipofariki kwa ajali ya gari pale Wami Dakawa, Morogoro.
Ninaamini aliteuliwa kwa vipindi viwili tofauti kutokana na imani kubwa aliyokuwa nayo Mheshimiwa Rais kwake. Imani hiyo inatokana na ukweli kuwa alikuwa mchapakazi kweli kweli, mwaminifu, mtetezi wa wanyonge na msimamizi wa kweli wa maendeleo ya Taifa hili.
Tunapomkumbuka siku ya leo, ni dhahiri tunakumbuka Mtu aliyejitolea kwa hali na mali kupambana na Ujinga, Maradhi na Umaskini. Alipigana kufa na kupona kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo.
Tunamkumbuka sana Mzee Sokoine kwa uchapaji kazi wake na utetezi wa Wanyonge.  Atakumbukwa milele kwa jinsi alivyokuwa tayari kutetea maslahi ya wanyonge na kusimamia ujenzi wa Uchumi wa Tanzania.
Atakumbukwa siku zote kwa juhudi zake za kujenga Jamii ambayo inachukia rushwa, Jamii inayochukia Wahujumu Uchumi na Jamii inayochukia Walanguzi. Alipambana na Watu ambao walikuwa wanahodhi bidhaa zisiwafikie Watu wa chini kwa bei halali. Ninakumbuka maneno yake aliyoyasema kwamba “Kama Serikali ilikuwa likizo sasa likizo imekwisha”. Kwa maana hiyo aliwabana Walanguzi na Wahujumu Uchumi na hatimaye wakasalimu amri. 
Marehemu Sokoine alikuwa muasisi wa Biashara huria Nchini wakati tukiwa kwenye itikadi ya ujamaa.  Aidha, alikuwa na wazo zuri la kuanzisha usafiri wa Daladala Dar es Salaam.  Wakati wake Mabasi makubwa ya Ofisini yalitumika kubeba Watu Jijini Dar es Salaam;
Kutokana na juhudi zake, ndiyo sababu kumbukumbu zake ziko katika maeneo mengi Nchini.  Moja ya kumbukumbu hizo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kilichokoMorogorokwa jina laSokoine University of Agriculture.  Marehemu Sokoine alikuwa mpenzi mkubwa wa Kilimo.  Alipenda Kilimo cha Plau na Matrekta ili kuondokana na Kilimo cha Jembe la Mkono.
Marehemu Sokoine alishiriki kuanzisha dhana ya Nguvu Kazi ili kumfanya kila Mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi kufanya hivyo.  Nakumbuka alitoa mshahara wake asilimia 50 kutunisha Mfuko wa Rais wa Nguvu Kazi.  Mfuko ambao ulisaidia Watu wa kipato cha chini;
Marehemu Sokoine alikuwa Kiongozi wa kipekee.  Tunamkumbuka kwa kile alichoamini kwamba “Uongozi ni Dhamana”. Kwa maoni yake aliamini kwamba, kuwajibika kama Kiongozi ni kukubali kwa hiari dhamana ya Uongozi unayopewa ama kwa njia ya kuomba kwa kura au kwa kuteuliwa Kikatiba au Kisheria. Aliamini kuwa Kiongozi lazima akubali kutumia dhamana ya uongozi aliopewa kwa maslahi ya umma na kwa Taifa kwa ujumla;
 
Kwa misingi hiyo, Marehemu Sokoine alikuwa mstari wa mbele kukubali Kanuni za Chama chake.  Aliamini kwamba Kiongozi hatatumia dhamana ya madaraka yake kujinufaisha mwenyewe binafsi au Mtu mwingine yoyote, bali Taifa zima;
Marehemu Sokoine aliamini kuwa Kiongozi daima atakuwa ni mtiifu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na atamshauri kwa hekima na kwa mujibu wa Sheria zilizowekwa;
Marehemu Sokoine, pamoja na kupenda kusimamia maendeleo ya Nchi yetu, pia alikuwa Mcha Mungu-Mtu wa Kiroho, mwenye kupenda Dini.  Mtu mwenye kupenda Watu.  Mtu wa Imani. Wote sisi ni mashahidi kwamba Marehemu Sokoine alikuwa Mtu wa Mungu na ili kudhihirisha hili siku aliyopata ajali alipita na kusali katika Kanisa hili kabla ya kuanza kwa safari ya kuelekea Dar es Salaam. Hiyo ilikuwa ibada yake ya mwisho akiwa hai kabla ya kufikwa na mauti.
Marehemu Sokoine atakumbukwa kwa mengi ambayo kwa kweli tukiyaongelea hapa hatutayamaliza;
 
Ninachoweza kusema, leo tunamkumbuka Mtu ambaye kwetu sisi Watanzania, ni kielelezo bora cha utumishi wa watu, kielelezo cha kujituma, kielelezo cha upendo, kielelelzo cha kupenda haki kielelezo cha kupigania wanyonge na kielelezo cha kumcha na kumtumikia Mungu
Marehemu Sokoine amefanya mengi mazuri ambayo tunayakumbuka leo. Hebu tujifunze kutoka kwake kwambaThe good we do today becomes the happiness of tomorrow” ikimaanishwa kwamba -Mazuri tunayoyafanya leo, huwa furaha ya kesho. Tumuige kwa kufanya mazuri ambayo yatakumbukwa daima na vizazi vijavyo.
Viongozi mliojumuika nasi hapa leo na
Ndugu Waumini;
Nimalizie kwa kuungana na Ndugu, Jamaa na Marafiki wote wa Familia ya Marehemu Mzee Edward Moringe Sokoine kuendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ili ampumzishe mahali Pema Mbinguni. Mungu ailaze Roho ya Marehemu Mahali Pema Peponi.   AMINA
imetolewa na ofisi ya waziri mkuu.

1 comment:

Anonymous said...

Mtoto wa mkulima anasema kwa uchungu na kuonyesha jinsi anavyomuenzi mtu aliekuwa mtu wa watu na asiependa makuu kama yeye!

Big UP PM